YOUTH TECHNOLOGY INITIATIVE

Friday, August 26, 2011

Dereva anayedaiwa kuua mbunge, mkewe ashtakiwa
HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Kitengo cha Mifupa (MOI), jumatano(tarehe 24) iligeuka kuwa mahakama kwa muda baada ya dereva wa aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Uzini, Chezard Sebunga (31), kusomewa mashtaka matatu akiwa chini ya ulinzi hospitalini hapo.

Sebunga, ambaye ni mkazi wa Dodoma na dereva wa aliyekuwa Mbunge wa Baraza la Wawakilishi (CCM), Mussa Silima, alisomewa mashtaka matatu likiwamo la kusababisha vifo vya watu wawili; mbunge na mkewe na kujeruhi abiria kutokana kuendesha gari kwa uzembe.

Sembunga anadaiwa kusababisha ajali hivi karibuni, eneo la Nanenane-Nzuguni barabara ya Dodoma Morogoro na kusababisha watu wawili kupoteza maisha na mwingine kujeruhiwa.
Mshtakiwa huyo amelazwa wodi maalumu chumba namba mbili, baada ya kuvunjika mguu wa kulia mara tatu na kuwekewa chuma.

Katika ajali hiyo, mshtakiwa anadaiwa akiendesha gari aina ya Toyota Coralla aligongana na lori, kisha kuhama njia na kugonga Scania lililokuwa upande wa pili wa barabara.

Alidaiwa kusababisha vifo na kuendesha gari kwa mwendokasi na kusababisha abiria Salma Juma kujeruhiwa.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Nassoro Katuga, alidai mshtakiwa alitenda makosa hayo Agosti 21, mwaka huu barabara ya Dodoma -Morogoro eneo la Nanenane Nzunguni, Manispaa ya Dodoma.

Mwanga alidai siku ya tukio saa 9:00 alasiri eneo hilo, akiwa na gari hiyo aina ya Toyota Corolla anadaiwa kuendesha gari kwa uzembe baada ya kushindwa kutumia tahadhari na kusababisha kifo cha Mwanaheri Mwaibu.
Aliendelea kuwa mshtakiwa akiwa dereva aliendesha gari kwa mwendokasi na uzembe bila tahadhari na kusababisha kifo cha Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Uzini, Mussa Silima.

Katika shtaka la tatu, mtuhumiwa siku na wakati huohuo anadaiwa kumjeruhi abiria, Salma Juma.
Mshtakiwa alikana mashtaka na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Joyce Minde, aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 8, mwaka huu itakapotajwa tena.Minde alisema mshtakiwa atafunguliwa mashtaka upya atakapopelekwa Dodoma.

No comments:

Post a Comment