YOUTH TECHNOLOGY INITIATIVE

Friday, August 26, 2011

Makinda ambana Waziri Muhimbili kukatiwa umeme
SPIKA wa Bunge Anne Makinda jana alimbana Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima akimtaka atoe maelezo ni kwa nini juzi umeme ulikatika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).Makinda alimtaka Naibu Waziri kutoa sababu za msingi za kukosekana kwa huduma ya umeme katika hospitali hiyo akisema ni jambo la hatari kwa afya za wagonjwa.

Juzi, iliripotiwa kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili haikuwa na huduma za umeme na maji jambo lililosababisha kero kwa wagonjwa na kukwamisha baadhi ya huduma muhimu.“Mheshimiwa Naibu Waziri, hebu eleza hata Muhimbili hakuna umeme wala maji, hilo nalo unawaambiaje Watanzania?’’ alisema Makinda.Swali hilo lilimpa wakati mgumu Malima kulijibu akisema hata yeye hajui sababu za taasisi hiyo nyeti kukatiwa umeme.

Malima alitaja sababu za Jiji la Dar es Salaam kukosa umeme kuwa ni pamoja na matatizo katika Gridi ya Taifa ambapo Megawati 150 zilikosekana katika siku za karibuni lakini akasema hicho siyo kigezo cha kuifanya Muhimbili ikatiwe umeme.

“Mheshimiwa Spika, nataka niseme hapa kuwa kwenye Gridi ya Taifa kulikuwa na tatizo lililolifanya Jiji likose umeme wa megawati 150 hivi, lakini hata hivyo, hiyo siyo sababu ya kufanya Muhimbili wakose umeme labda kuna tatizo jingine naomba unipe muda nifuatilie nitatoa jibu la uhakika,’’ alisema Malima.

Naibu Waziri alisema tatizo kubwa katika hospitali hiyo halikutokana na uzalishaji, bali alihisi kuwa vipo vyanzo vingine ambavyo hata hivyo hakuweza kuvibainisha.


Hali ya Muhimbili
Leon Bahati na Godfrey Nyang’oro, wanaripoti kuwa huduma kwa wagonjwa wanaotibiwa na kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili imezorota kutokana na kukatika na umeme mara kwa mara kwa siku ya tatu mfululizo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wauguzi, wagonjwa na waganga wa wadi za Mwaisela na Sewa Haji, katika hospitali hiyo walisema kwamba, hali ni mbaya zaidi katika wadi za wagonjwa ambazo hazipati umeme wa jenereta.

Mmoja wa wauguzi ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa kuhofia ajira yake alisema kuwa, wodi ya Sewa Haji ipo giza badala yake wanatumia taa za chemli na kwamba, kutokana na hali hiyo wanapata wakati mgumu kukabiliana na msongamano wa wagonjwa.

Muuguzi huyo alisema tangu ulipoanza kukatika umeme siku mbili zilizopita, maeneo yote ya wodi hayana umeme. “Mapokezi na maabara wanatumia umeme wa jenereta na wodini hakuna, tunatumia taa za kawaida,” alifahamisha muuguzi huyo.

Mwananchi lilipotembelea Muhimbili lilishuhudia mafundi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) wakiendelea na ukarabati wa nyaya katika baadhi ya maeneo.

Ofisa Uhusiano wa Taasisi ya Mifupa (Moi), Almasi Jumaa, alisema kwamba kwa upande wa taasisi hiyo hali ni shwari kwa sababu wana jenereta za kutosha ambazo huzitumia umeme wa Tanesco ukikatika.

"Hatuna tatizo kwa upande wa Moi. Sisi kama taasisi inayojitegemea tuna jenereta ambazo wakati wote ziko tayari kufanya kazi mara umeme unapokatika," alisema Almasi.

Ofisa Habari wa MNH, Aliamini Aligaesha, alikiri hospitali hiyo ilikosa umeme kwa siku tatu mfululizo kutokana na matatizo ya kiufundi kwenye mtandao wa usambazaji ndani ya hospitali hiyo.

Alisema kwamba, siyo kawaida kwa hospitali hiyo kupata mgawo wa umeme tangu matatizo ya nishati hiyo yalipoanza nchini, lakini kwa siku tatu hali ilikuwa mbaya.

Alisema waliweza kukabiliana na tatizo hilo kwa kuwasha jenereta isipokuwa wodi tatu za Sewahaji, Mwaisela na Kibasila, ambazo hazina jenereta hivyo zilibakia gizani na kwamba badala yake watumia taa za chemli na zinazotumia umeme wa kuchaji.

Aligaesha alifahamisha kuwa umeme ulikatika Jumatano iliyopita na mafundi wa Tanesco na MNH wanashirikiana kutatua tatizo hilo.

" Hapa umeme ulikatika Jumatano saa 1:00 jioni. Tuliwaita Tanesco, walipofika waligundua hitilafu ya umeme kwenye njia kubwa wakairekebisha. Ilipokamilika tukaunganisha, lakini baadaye tukagundua kuna tatizo upande hospitali," alisema Aligaesha.

Aliwatetea mafundi wa Tanesco kwamba huwa wanatoa ushirikiano wa hali ya juu kutatua tatizo la umeme kila linapotokea hospitalini hapo, lakini hilo limeonekana kuwa zito na linahitaji umakini zaidi.

Alisema menejimenti ya MNH inajitahidi kukabiliana na tatizo hilo kwa kununu jenereta maalumu kwa ajili ya majengo hayo matatu.

"Unajua Muhimbili tuna majengo karibu 20 na yote yanahitaji kuwa na jenereta. Hata hizo wodi tatu tunaamini baada ya muda yatawekea jenereta," alisema Aligaesha.


No comments:

Post a Comment