Gaddafi atoa ujumbe akiwa mafichoni, vikosi vyake vyajibu mapigo
TRIPOLI, Libya
VIKOSI vya jeshi vinavyomtii Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, jana vilikutana uso kwa uso na kupambana vikali na vikosi vya waasi na vile vya Umoja wa Kujihami Nchi Magharibi (Nato).
Gaddafi, ambaye anatafutwa na waasi kwa nguvu zote, juzi walitangaza zawadi ya dola 1.7 milioni za Marekani (Sh2 bilioni) kwa mtu yeyote atakayewezesha kukamatwa, au kumuua Gaddafi.Habari zinasema Gaddafi alitoa ujumbe akiwa mafichoni akivitaka vikosi vyake vyote vya jeshi, ambavyo vilipunguza kasi ya kupigana vijibu mashambulizi waliopo mjini Tripoli.
Vikosi hivyo vinavyomtii Gaddafi katika hatua ya kuurudisha uwanja wa ndege wa kimataifa unaoshikiliwa na waasi, jana vilipigana vikali na waasi kwenye uwanja huo ambao ndiyo mkubwa nchini humo.
Hata hivyo, waasi hao bado wanajigamba kuwa mji wa Tripoli tayari wameudhibiti. Usiku wa kuamkia jana milio ya risasi na milipuko ya mabomu ilitikisa mji wa Tripoli hasa uwanja huo wa ndege, ambao mpaka hivi sasa unashikiliwa na waasi.
Nato walenga handaki la Gaddafi
Wakati Gaddafi anatoa ujumbe wa kuendeleza mapambano, ndege za Nato jana zilishambulia kwa kurusha mabomu kwenye handaki kubwa lilikopo mji wa Sirte, alikozaliwa kiongozi huyo.
Ndege hizo ziliondoka kambi ya jeshi iliyopo Nolfolk siku ya Alhamisi usiku.Hata hivyo, waasi wa Libya nao wanaimarisha majeshi yao kwenye barabara inayoelekea Sirte, wakipeleka vifaru na makombora.
Wakati huohuo, Umoja wa Ulaya (EU) umesema utapeleka misaada ya haraka ya dawa kwenye hospitali zilizofurika wagonjwa, ambako hali inaarifiwa kuwa mbaya.
Waasi wahamia Tripoli
Baraza la Mpito la Kitaifa la limeondoka Benghazi na kuhamia Tripoli. Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji, Ali Tahuni, alisema baraza hilo limeanza kufanya kazi mjini humo.Baraza la Mpito la Kitaifa, limeahidi kuwasamehe wanajeshi na wanamgambo waliokuwa wakimpigania Gadaffi, ikiwa wataweka silaha chini.
Gaddafi bado yupo mafichoni
Bado haijulikani mahali alipo Kanali Gaddafi na familia yake. Katika hatua nyingine, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, amezishutumu nchi za Magharibi kwa kukiuka azimio la Umoja wa Mataifa dhidi ya Libya.Kwa upande mwingine bila ya kujali iwapo Kanali Gaddafi atakamatwa au la, mkutano wa kimataifa kwa ajili ya kujenga upya Libya umepangwa kufanyika Septemba Mosi.
Naye Msemaji wa waasi, Abdel Salam Abu Zaakouk, alisema mazungumzo yanaendelea kati yao na viongozi wa makabila maeneo mbalimbali kutafuta suluhu ya mzozo huo.
Alisema uongozi wa waasi uliahidi kukubali Kanali Gaddafi aondoke salama nchini humo kwa kuachia madaraka.
Lakini, kiongozi huyo wa Libya ambaye hajulikani aliko aliapa kupitia hotuba iliyorushwa kupitia redio moja ya kitaifa kwamba, yuko tayari kupigana hadi ashinde au afe.
UN yaidhinisha fedha
Umoja wa Mataifa (UN) umetoa idhini ya kuziachia dola 1.5 bilioni za Gaddafi zilizozuiliwa. Fedha hizo zitatumiwa kwa misaada ya kiutu kwa nchi hiyo iliyokumbwa na mapigano.
Kwa mujibu wa uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, fedha hizo zinatazamiwa kusaidia Serikali kujenga upya Libya kufuatia mapigano ya miezi kadhaa.
No comments:
Post a Comment